![]() |
| Kocha wa Timu ya Taifa ya Tanzania Charles Boniface Mkwasa |
Kocha wa timu ya Taifa ya Tanzania Taifa Stars Charles Boniface Mkwasa atajikuta katika wakati mgumu baada ya kuwatuhumu wananchi wa Algeria kuwa ni wabaguzi wa rangi.
Mwenyekiti wa Chama cha Wanasoka wa Algeria, Ahmed
Boudry ameamua kumfungulia mashitaka Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Charles
Boniface Mkwasa.
Kulingana na habari kutoka kwenye tovuti ya Le Buteur, Boudry
amesema wamekerwa kupita kiasi na kauli ya Mkwasa kwamba raia wa
Algeria ni wabaguzi wakubwa wa rangi, hivyo wameamua rasmi kumfungulia mashitaka katika
Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).Ahmed Boudry alisema kuwa nanukuu.
“Mkwasa aliyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari hata kabla ya mechi ambayo Tanzania ilifungwa bao saba. Tunaamua kumfikisha Fifa kwa kuwa amewadhalilisha raia wote wa Algeria wakiwemo wachezaji".
Pia aliongeza kuwa:-
“Mkwasa hakuwa na ushahidi, Tanzania imekuja hapa zaidi ya mara moja na hatujawahi kupata malalamiko ya ubaguzi wa rangi, vipi yeye Mkwasa aseme hayo?” alihoji kiongozi huyo.
Kabla ya kauli yake hiyo, vyombo vingi vya habari vya Algeria vilizungumzia suala la Mkwasa kusema Waalgeria ni wabaguzi wa rangi. Vyombo hivyo vya habari vya Algeria ikiwemo mitandao inayotumia lugha ya Kifaransa vilimshambulia Mkwasa kwa madai amewakashifu Waalgeria.
Algeria iliing’oa Stars kwa kuifunga mabao 7-0 katika mechi ya marudiano kufuzu Kombe la Dunia 2018 mjini Bilda. Stars imeaga michuano hiyo kwa kufungwa jumla ya mabao 9-2 kwani awali ilitoka sare ya mabao 2-2 jijini Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Taifa.

No comments:
Post a Comment