Saturday, 14 November 2015

Saturday 09:42 PM

Hadi mwamuzi anapuliza kipyenga cha mwisho kuashiria kuisha kwa mchezo kati ya Taifa Stars na Algeria ubao wa matokeo ulikua ukisomeka Taifa Stars 2-2 Algeria, sare hii inaiweka Taifa Stars katika mazingira magumu ya kuweza kufuzu kwa hatua inayofuata ambayo ni hatua ya makundi, kwani itahitajika kupata ushindi au Sare ya magoli zaidi ya mawili katika mchezo wa marudiano utakaochezwa huko Algeria mapema mwaka huu.

Katika mchezo huu wa kwanza uliochezwa katika uwanja wa Taifa Dar-es-Salaam huku ukiudhuriwa na maelfu ya Watanzania wakiongozwa na Rais mpya wa Awamu ya Tano Mh. Dr. John Pombe Magufuli ambaye alikua ni mgeni rasmi katika pambano hilo huku akisindikizwa na Rais aliyemaliza muda wake Dr. Jakaya Mrisho Kikwete, Taifa Stars ilionekana kukianza kipindi cha kwanza cha mchezo huo vyeema na kwa kasi kubwa huku kukiwa na kosakosa za hapa na pale kutoka kwa washambuliaji wake wakiongozwa na mchezaji wa kulipwa Mbwana Sammata, Thomas Ulimwengu na Farid Musa ambao kwa nyakati tofauti tofauti walilitia lango la Algeria  katika wakati mgumu. Taifa Stars katika kipindi cha kwanza ilioneka kuishika Algeria haswa katika eneo la kiungo ambapo waliongozwa na Himidi Mao Mkami na Mudathiri Yahaya ambao walicheza kwa uelewano wa hali ya juu.

Taifa Stars iliendelea kulisakama lango la Algeria kwa kasi ya hali ya juu hadi mnamo dakika ya 43 ya mchezo ambapo mshambuliaji Elius Maguli aliweza kuwainua mashabiki wote waliojitokeza kushuhudia mchezo huu katika viti vyao alipoiandikia Taifa Stars Goli la kwanza baada ya kupokea krosi safi kutoka kwa winga Farid Mussa, hadi kipyenga kinapulizwa kuashiria mapumziko ubao ulisomeka Taifa Stars 1-0 Algeria.

Kipindi cha pili kilianza kwa Algeria kufanya mabadiliko katika eneo lao la kiungo kwa kumuingiza Bintaleb Nabil kiungo anayesakata kandanda katika klabu ya Tothnam Hotspurs ya pale Uingereza ambaye alileta matumaini kiasi kwa upande wa Algeria, lakini katika dakika ya 56 mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania Mbwana Ally Sammata aliiandikia Taifa Stars bao la pili baada ya kuichambua vilivyo safu ya ulinzi ya Algeria na kufanya ubao usomeke Taifa Stars 2-0 Algeria.

Kocha wa Timu ya Taifa Charles Boniphass Mkwasa Master alifanya mabadiliko kwa kumpumzisha kiungo Mudathiri Yahaya na mshambuliaji Elius Maguli na nafasi zao kuchukuliwa na Said Ndemla na Mrisho Khalifani Ngassa lakini mabadiliko haya hayakuwa msaada kwa Taifa Stars kwani mnamo dakika ya  71 mshambuliaji wa Algeria Sliman Islam aliweza kuiandikia Algeria goli la kwanza huku akiwaacha mabeki wa stars wakidhania alikua offside, goli hili lilionekana kuwapa nguvu Algeria ambao hazikuwachukua dakika mbili kusawazisha na goli la pili na kufanya ubao usomeke Taifa Stars 2-2 Algeria.

@Elirinyo

No comments:

Post a Comment